Abstract
Vyombo vya habari vya Kichina vimekuwapo katika eneo la Afrika Mashariki
tangu miaka ya 1960. Redio China Kimataifa (CRI) ilianza matangazo yake kwa
lugha ya Kiswahili nchini Tanzania mnamo Septemba 1961. Ili kupata wafanyakazi
wa Kichina walio na uwezo wa Kiswahili, lugha ya Kiswahili ilianza kufundishwa
kama somo katika Chuo cha Utangazaji cha Beijing. Hadi sasa idhaa ya Kiswahili
ya CRI inatangaza katika lugha ya Kiswahili. Wasimamizi wengi wa idhaa hii ni
Wachina na wanakimudu Kiswahili vilivyo. Katika miaka ya hivi karibuni,
hususani kuanzia mwaka 2011, vyombo vya habari vya Kichina vinavyotangaza
katika lugha ya Kiswahili vimeongezeka. Baadhi ya hivi vyombo ni Shirika la
Habari la Xinhua (Kupitia runinga yake ya CNC mtandaoni), shirika la runinga
la CCTV (mtandaoni) na kampuni ya usambazaji wa mawimbi ya StarTimes.
Tangu ongezeko hili lishuhudiwe, hakujakuwapo na utafiti wa kuonesha ni kwa njia
gani vyombo hivi vimechangia katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili.
Makala hii ililenga kufafanua ni kwa njia gani vyombo vya habari vya Kichina
vimechangia katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Ili kufanikisha lengo
hili, mbinu mbalimbali za utafiti zilitumiwa. Makala mbalimbali zilisomwa na
kuchanganuliwa kwa kina. Vilevile, vipindi na matangazo kadhaa
yanayopeperushwa katika vyombo hivi yalichanganuliwa. Mwishowe, wafanyakazi
wa baadhi ya vyombo hivi walihojiwa. Matokeo ya utafiti huu yaliwasilishwa kwa
njia ya ufafanuzi.
This work is licensed under a Creative Commons Attribution 4.0 International License.
Copyright (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU