Abstract
Hadhi ya Kiswahili katika eneo la Afrika Mashariki inatofautiana katika mataifa
tofauti. Nchini Kenya, Kiswahili ni lugha rasmi na pia lugha ya taifa. Nchini
Tanzania, ni lugha ya taifa na pia hutumika katika shughuli nyingi rasmi. Ndiyo
lugha itumiwayo katika kiwango cha elimu ya msingi. Nchini Uganda, Kiswahili
kimeteuliwa kama somo la lazima katika mtaala uliozinduliwa mnamo mwaka
2017. Kilipendekezwa kama lugha rasmi ya pili ya Uganda mnamo mwaka 2005
lakini pendekezo hilo halijapitishwa rasmi. Mnamo mwaka 2017, Bunge la Chini
la Rwanda lilipitisha sheria inayotambua Kiswahili kama lugha rasmi nchini humo.
Makala haya yanatumia nchi hizi nne za Afrika Mashariki kuchunguza maendeleo
ya Kiswahili katika kipindi cha sasa na kuonesha kama maendeleo hayo yana
matokeo chanya au hasi katika mataifa husika na eneo lenyewe. Utafiti utaongozwa
na nadharia iliyoasisiwa na Howard Gile ya Makubaliano ya Mawasiliano (CAT)
lakini ambayo imeendelezwa katika hali nyingi. Yatatumia mihimili yake ya
mwachano na makutano. Makala yanachukulia kwamba maendeleo ya sasa ya
Kiswahili yana manufaa mengi kuliko hasara.
This work is licensed under a Creative Commons Attribution 4.0 International License.
Copyright (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU