Muhtasari
Mzunguko wa Ukanushi wa Jespersen ni mfuatano wa michakato katika Isimu
Historia ambao huelezea maendeleo ya kihistoria ya ukanushi katika lugha
mbalimbali unaojenga mzunguko. Kwa kuwa Mzunguko wa Ukanushi wa Jespersen
(MUJ) bado haujatazamwa katika lugha ya Kiswahili, makala haya yanakusudia
kuziba pengo hilo. Makala haya ni matokeo ya uchambuzi wa mapitio ya maandiko
mbalimbali yahusuyo ukanushi. Baadhi ya mifano ya tungo za ukanushi ni kutoka
kwa mwandishi kutokana na tajiriba na utaalamu alionao katika isimu ya lugha ya
Kiswahili na Kiingereza. Tajiriba hii inatokana na ufundishaji wa kozi za mofolojia
na fonolojia kwa takribani miaka sita. Moja ya mapitio ya msingi ni Ashton (1944)
japo yeye na wengine waliomfuata hawakugusia suala la MUJ. Makala haya
yamebainisha kuwa katika lugha ya Kiswahili, MUJ ni vigumu kubainishwa
kihistoria/kidaikronia kama ilivyobainishwa na Jespersen. Akitumia mfano wa
lugha ya Kifaransa, kabla ya lugha hiyo haijasanifishwa kulikuwa na umbo moja la
ukanushi ne lililokuwa likijitokeza kabla ya kitenzi, baada ya lugha hiyo
kusanifishwa; umbo lingne la ukanushi pas liliongezeka mwishoni mwa kitenzi na
baadaye Kifaransa cha mitaani kiliibuka huku kikipuuza kutumia kikanushi ne,
hivyo, kurudi tena katika mfumo wa ukanushi wa mwanzo wa tungo kuwa na
kikanushi kimoja. Mtiririko huu ulionekana kujenga hali ya mzunguko/uduara.
Makala haya yamebainisha kwamba suala hilo katika Kiswahili hujitokeza
kisinkronia kwa kuutazama ukanushi kwa jinsi ulivyo kwa wakati wa sasa
(kipindi hiki cha miaka ya 2000) katika Kiswahili. MUJ katika Kiswahili
hujitokeza katika misingi kwamba baadhi ya vitenzi vina umbo moja la ukanushi
wakati vitenzi vingine vina maumbo mawili. Kimantiki, tungo hizo zenye maumbo
mawili ya ukanushi zinaonesha kuwa na dhana ya maana ya ukanushi moja na siyo
mbili ndani ya kitenzi kimoja. Kwa hivyo, vinaleta hali ya mzunguko kwa maana
ya kwamba kumekuwa na ongezeko la kikanushi cha pili lakini dhana ya maana
ya ukanushi imerudi kuwa moja sawa na vitenzi vyenye kikanushi kimoja.
Kazi hii imewekwa chini ya Leseni ya Creative Commons Kutambulisha 4.0 Kimataifa.
Hakimiliki (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU