Muhtasari
Mwingilianomatini ni hali ya kazi mbili au zaidi za fasihi kuingiliana. Mwingiliano
huu waweza kutokea kisadfa ama waweza kuwa umetokea ili kutimiza matakwa
fulani ya mtunzi. Mwingilianomatini huweza kutokea katika vipengele mbalimbali
vya kazi zinazohusika hususan katika: muundo, msuko, uumbaji wa wahusika na
uhusika, mtindo, masuala yanayoshughulikiwa miongoni mwa mambo mengine.
Makala haya yanalenga kujadili hali ya kuingiliana inayojitokeza kati ya tamthilia
ya Kilio cha Haki (A. Mazrui) na Kigogo (P. Kea). Utafiti awali unaonesha kuwa
tamthilia hizi mbili zinaingiliana katika vipengele vingi mathalani: usawiri wa
wahusika na uhusika, muundo, na msuko wa vitushi kati ya mambo mengine. Hata
hivyo, uchunguzi utajikita zaidi katika kutalii suala la usawiri wa mwanamke.
Lengo la makala haya ni kutathmini mwingiliano uliopo kati ya tamthilia hizi mbili
ili kufafanua namna tamthilia hizi zinavyojengana na kukamilishana katika
kusawiri masuala ya jinsia ya kike. Je, kuna mwingilianomatini katika kusawiri
masuala ya wanawake katika tamthilia ya Kigogo na ile ya Kilio cha Haki? Kazi
hizi mbili zimechanganuliwa kwa mwongozo wa mihimili ya Nadharia ya
Mwingilianomatini.
Kazi hii imewekwa chini ya Leseni ya Creative Commons Kutambulisha 4.0 Kimataifa.
Hakimiliki (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU