Muhtasari
Ngano ni sanaa ya usimulizi ya Kiewe ambapo usimulizi, utendaji na ubunifu
zinaungana pamoja katika mfumo wa kifasihi na mtu mmoja au kundi la watu.
Tunasema mtu mmoja kwa maana ya kuwa baadhi ya mbinu zinazotumika
zinategemea uwezo wa kifasihi wa msimulizi. Vilevile, zinaweza kuwa kwa kundi
la wasimulizi kwa sababu baadhi ya mbinu zinazotumika ni kutoka katika jamii
na zinagunduliwa pamoja na jamii. Utanzu wa ngano (ambao kwa Kiewe ni Gli)
huchukuliwa na Waewe kuwa ni usimulizi wa mdomo unaotumia mbinu za kifasihi
za kuwakilisha tamaduni na maisha ya jamii hiyo. Kumbo hii ya fasihi simulizi
inatumika kuelimisha jamii ambayo inakuwa katika mfumo wa kuchanganya
maadili, mafunzo na burudani kwa pamoja. Maudhui muhimu katika Gli ni
kukemea tabia mbaya, ambayo haikubaliki katika jamii, na kuhimiza tabia njema,
zinazokubalika katika jamii inayohusika. Hali kadhalika, ngano hutumika
kuwatia moyo wanajamii katika shida na matatizo mbalimbali. Ngano nyingi
hutumia mbinu mbalimbali za kifani katika uwasilishaji wa maudhui yake.
Miongoni mwa mbinu maarufu zinazotumiwa na ngano ni matumizi ya motifu, na
hasa motifu ya safari ya msako. Motifu hii hutumiwa kuwahamasisha wanajamii
kujitafutia maisha mazuri kupitia safari ya msako. Aidha, hutumika kuibua
maadili mbalimbali muhimu kwa jamii hii. Katika makala haya, tunajaribu
kuwasilisha namna ngano za Kiewe zinavyoonesha utofauti katika ruwaza ya shujaa
kwa mujibu wa Campbel. Kwa kuzungumzia suala hili, makala haya yamezingatia
masimulizi ya ngano za Kiewe yenye motifu ya safari ya msako.
Kazi hii imewekwa chini ya Leseni ya Creative Commons Kutambulisha 4.0 Kimataifa.
Hakimiliki (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU