Muhtasari
Lugha huingiliana na kuathiriana zaidi zinapotumiwa katika mazungumzo katika
eneo mahususi la kijiografia. Mwingiliano wa lugha hujitokea katika viwango anuwai
vya kiisimu mojawapo ikiwa mwingiliano wa maneno kati ya L1 na L2. Makala
haya yameshughulikia matokeo ya utafiti kuhusu uchanganuzi wa mwingiliano wa
maneno katika mazungumzo kwa Kiswahili kati ya lugha ya Kigisu na Kiswahili
nchini Uganda. Utafiti huu ulitokana na tafiti za hapo awali zinazoripoti kwamba
lugha ya kwanza huathiri umilisi wa lugha ya pili katika nyanja mbalimbali za
kiisimu. Kwa hiyo, makala haya yanaripoti kuhusu matokeo ya matumizi ya maneno
ya vitenzi na nomino miongoni mwa wanafunzi wanaojifunza na kuzungumza
Kiswahili kama lugha ya pili ili kubainisha jinsi lugha ya Kigisu inavyoathiri lugha
ya mazungumzo kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili kama
lugha ya pili. Nadharia za Mwingiliano Lugha ya Selinker (1972), na Uchanganuzi
Makosa kama inavyoelezwa na Lennon (2008) zilitumika kubainisha athari za
mwingiliano wa maneno kati ya L1 na L2. Data ilikusanywa kutoka kwa
wanafunzi 78 wa kidato cha tatu miongoni mwa wanafunzi wa shule nne za upili
wanaoongea Kigisu kama L1 na ambao ni wanafunzi wa lugha ya Kiswahili.
Matokea ya utafiti yanadhihirisha ujumuishaji wa nomino na vitenzi katika
mazungumzo kwa Kiswahili, uhamishaji wa nomino na vitenzi kutoka L1 kwa L2
na ubadilishanaji wa nomino na vitenzi vya Kiswahili na vile vya Kigisu katika
mazungumzo.
Kazi hii imewekwa chini ya Leseni ya Creative Commons Kutambulisha 4.0 Kimataifa.
Hakimiliki (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU