Muhtasari
Kikwazo cha lugha katika ufahamu wa masuala nyeti ya kitaifa au hata kimataifa
huweza kuharibu mawasiliano nchini na kusababisha kutoelewana miongoni mwa
watu. Aidha, kikwazo hicho kinaweza kukwamisha juhudi za maendeleo katika
taifa au hata kuzuia wananchi kuelewa yale yanayojiri katika nyanja za kimataifa.
Kikwazo hiki hutokea pale ambapo lugha moja rasmi ndiyo inayotumiwa hata kama
kuna lugha mbili rasmi, kuunda sera za nchi, kufafanulia mikataba na
makubaliano ya kitaifa na kimataifa au hata kuelezea sheria za nchi. Nchini Kenya,
wananchi wengi hawafahamu sera za nchi au hata Katiba ya Kenya. Hii ni kutokana
na hali kwamba Kiingereza ndicho kinachotumiwa kuunda sera, kuandikia Katiba
ya nchi, mbali na kuhifadhi mikataba na makubaliano yoyote rasmi yawe ni ya
kitaifa au kimataifa. Je, nafasi ya Kiswahili katika kuwafahamisha wananchi yale
yanayojiri nchini mwao iko wapi? Makala yanajadili kikwazo cha lugha katika
ufahamu wa masuala nyeti, sera au hata miradi ya kitaifa au kimataifa
inayotekelezwa nchini na jinsi masuala hayo yanavyoathiri wananchi walio wengi.
Udurusu wa baadhi ya mikataba, sera, sheria na makubaliano ya kitaifa na
kimataifa umefanywa ili kuonesha jinsi yasivyoeleweka au kufahamika miongoni
mwa Wakenya wengi. Makala yanapendekeza mikakati ya kuzingatiwa ili
kuwahusisha wananchi wote kama washiriki katika mambo yanayowaathiri na
kuweza kuchangia katika mijadala ya kitaifa na kimataifa inayoathiri maisha yao.
Kazi hii imewekwa chini ya Leseni ya Creative Commons Kutambulisha 4.0 Kimataifa.
Hakimiliki (c) 2024 JARIDA LA CHAUKIDU