Tunasikitika kwamba toleo hili la CHAUKIDU halikuweza kutoka kwa wakati uliotarajiwa kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu. Tunajua kwamba ni toleo lililosubiriwa na wengi kwa hamu kubwa. Kwa hivyo, tunawaomba wadau wetu wote wakiwemo waandishi wa makala na wasomaji watuwie radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza. Ushirikiano wa wataalamu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia ni muhimu kwa taaluma za Kiswahili ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa lugha ya Kiswahili na kuenea kwake duniani. Katika Kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwishoni mwa mwaka wa 2017, wadau kutoka sekta mbalimbali walishiriki na kujadili mchango wa kila tasnia katika kukiendeleza na kukiimarisha Kiswahili. Kongamano lilijadili jinsi kila tasnia ilivyochangia na inavyoendelea kuchangia kwa namna tofautitofauti ukuzaji wa lugha ya Kiswahili na jinsi ambavyo Kiswahili kilichangia na kinaendelea kuchangia kustawisha tasnia husika. Mawasilisho, mazungumzo, na mijadala iliyofanyika iliwasaidia washiriki kuanza kutafakari juu ya uundaji wa dira ya ukuzaji endelevu wa Kiswahili na ustawi endelevu wa jamii katika karne ya 21 kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Matokeo ya mijadala yote hiyo ni toleo hili la pili la CHAUKIDU ambalo linajumuisha mawazo ya wadau mbalimbali kupitia mawasilisho yaliyoangazia vipengele mbalimbali kama vile fasihi, isimu, nafasi ya vyombo vya habari katika ukuaji wa Kiswahili na ufunzaji na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Katika toleo hili, mada mbalimbali zimeshughulikiwa na waandishi kutokana na tafiti zao za uwandani na mapitio ya maandishi maktabani na kwingineko. Kimsingi basi, kuna makala mengi ambayo yamechapishwa katika toleo hili kuchangia hazina kubwa ya lugha ya Kiswahili. Kazi zilizochapashwa katika toleo hili ni zile zilizoitikia mwito wa mada kuu ya mkusanyiko wa wataalamu mbalimbali kuhusu Dira ya Karne ya 21– Ukuaji wa Kiswahili na Ustawi wa Jamii.