About the Journal

Jarida la CHAUKIDU ni jarida la kitaaluma linalochapishwa na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) na kusambazwa katika nakala ngumu na nakala-pepe. Jarida hili ni la kitaaluma na huchapishwa mara moja kwa mwaka katika lugha ya Kiswahili. Jarida hili huchapisha makala juu ya taaluma za Kiswahili ambazo hazijachapishwa kwingine wala hazijawasilishwa kuchapishwa katika jarida jingine au machapisho mengine.  Makala za jarida hili zitatathminiwa  kwa kufichisha (tathmini-fiche) ambapo watakaotathmini hawatamjua mwandishi wa makala. Jarida hili linapatikana katika tovuti ya chama.

Malengo

Lengo kuu ni kuwahusisha na kuwashirikisha wanazuoni wa na wapenzi wa lugha ya Kiswahili duniani kote katika kubadilishana maarifa na maoni. Ukuaji na usambaaji wa Kiswahili, na hadhi mpya inayopata Kiswahili inakuza haja ya wataalamu wa Kiswahili kujadili na kupashana maarifa kwa mapana zaidi. Kwa kuwaunganisha wataalamu wabobezi na wale wanaoibukia jarida linakusudia kuwajengea wanataaluma hao utamaduni wa kuandika na kubadilishana mawazo kitaalamu katika viwango vya kimataifa. Mchango mmoja wa jarida hili ni kuimarisha ushiriki wa wataalamu wa Kiswahili katika midahalo, malumbano na ukuzaji wa maarifa ya Kiswahili kimataifa.

 Jarida hili litapokea michango ya kitaaluma kutoka mikabala mbalimbali ya kinadharia na kimethodolojia.

Upeo

Jarida hili litachapisha makala za kitaalamu za fasihi, isimu, na utamaduni wa Kiswahili. Taaluma mbalimbali katika tanzu za kimapokeo na pia tanzu mpya zinazoibuka hasa kutokana na maendeleo ya teknolojia.

  1. Ufundishaji wa lugha
  2. Isimu: km fonetiki, fonolojia, mofolojia, semantiki, isimu linganishi, isimu jamii, nk
  3. Fasihi: fasihi simulizi, fasihi andishi,
  4. Ulinganifu wa Kiswahili na lugha nyingine za Afrika.
  5. Utamaduni wa Waswahili na wazungumzaji wa Kiswahili
  6. Sera na matumizi ya lugha
  7. Maendeleo ya Kiteknolojia

Aina za makala 

Tunatoa mwito kwa makala mbalimbali na tunapokea makala wakati wowote ule. Makala zitakazopewa kipaumbele ni:

  1. Makala za utafiti zenye kuonesha matokeo ya uchunguzi, midahalo, n.k
  2. Tahakiki za kazi za fasihi, sanaa na kazi nyinginezo
  3. Makala zanazoelezea na kufafanua mbinu za ufundishaji ujifunzaji wa lugha
  4. Makala kuhusu uundaji wa istilahi za Kiswahili
  5. Makala kuhusu maendeleo ya teknolojia na lugha ya Kiswahili

Miswada yote izingatie matakwa na mapokeo ya kiutafiti na kiuandishi kama yalivyoelekezwa katika tovuti hii.

Maelekezo kwa Uaandaaji wa Mswada

  • Miswada iandikwe katika mfumo wa MS Word na kuwasilishwa kwa wahariri kwa kutumia mfumo maalumu upatikanao katika tovuti yetu. Tuma Mswada kwa Kubofya Hapa.
  • Mswada mzima uandikwe kwa hati ya Garamond.
  • Isipokuwa tu maeneo machache ambayo utapewa maelekezo mahususi, aya zote ziandikwe kwa ukubwa wa pt. 11.
  • Pambizo ziwe na pt. 1 kwa upande wa juu na upande wa chini. Pambizo ziwe na pt. 1.5 kwa upande wa kushoto na kulia.
  • Ili kusaidia tathmini-fichishi, wasilisha mswada wako bila kuweka jina lako, wala vidokezo vyovyote vya majina ya waandishi, taasisi wanakofanyia kazi, anuani-pepe zao, na nambari za ORCID kama wanazo. Makala ambazo hazitazingatia maelekezo haya, zitakataliwa na hazitafanyiwa tahakiki.
  • Taarifa kuhusu mwandishi/waandishi wa mswada, lazima zijazwe katika fomu maalumu ya kupokelea makala.
  • Mswada ifanyiwe uhariri wa kina kabla ya kuwasilishwa katika jarida.
  • Urefu wa mswada uwe ni maneno kati ya 3000 na 7000. 
  • Anuani ya mswada na vichwa vya sehemu zote za mswada viandikwe kama vinavyoonekana katika Sampuli ya Mswada.
  • Ikisiri: Ikisiri isizidi maneno 250. Ikisiri isiwe na tanbihi za chini ya ukurasa wala isiwe na marejeleo.
  • Chini ya ikisiri paandikwe maneno muhimu ya makala/mswada.
  • Marejeleo: Tumia mtindo wa APA toleo la 7. Unaweza kupata maelezo kuhusu APA kwa kutumia kiungo Hiki Hapa.
  • Usitumie tanbihi isipokuwa tu pale ambapo kuna ulazima huo. Tanbihi, ikiwa itatumiwa iwe kama ifuatavyo: Tumia fonti ya 10 pt na tanbihi zitambulishwe kwa tarakimu 1, 2, 3, nk.
  • Nukuu: Data na maneno kutoka lugha nyingine yaandikwe kwa italiki. Tafsiri za maneno ya kigeni ziwe katika alama za nukuu moja (`) na alama za nukuu mbili (“) zitatumika kuonesha nukuu za aina nyingine.
  • Maelezo zaidi yanapatikana katika Sampuli ya mswada wa awali